Je, manjano ni tiba ya miujiza au imani tu?
Je, manjano ni tiba ya miujiza au imani tu?
Iwe unapika rojo ya kuku ya Kihindi, biriani ya nyama ya ngamia ya Sudan, laksa ya Malaysia au macher jhol ya Bangladesh, vyote vina kitu kimoja cha msingi, manjano.
Lakini mbali na kuboresha ladha ya chakula, je, manjano ambayo ni moja ya viungo vya kale na vinavyopendwa zaidi duniani, yanaweza pia kuleta faida kubwa kwa afya zetu?
Akizungumza na kipindi cha Food Chain, Ragini Kashyap, mtafiti wa masuala ya chakula na mtayarishaji wa podikasti anayechunguza vyakula vya Kusini mwa Asia, alisema: "Familia yangu ina asili ya Punjab na siwezi kufikiria chakula chochote ambacho hatutumii manjano."
Kuna takriban aina 30 za manjano. Hutumika sana katika mapishi ya Asia, Afrika, na Amerika Kusini.
Hata hivyo, kwa sasa manjano hutumika katika sehemu nyingi duniani, kuanzia visiwa vya Pasifiki kama Bali na Fiji upande wa mashariki hadi eneo la Karibea upande wa magharibi,kutokana na uhamiaji wa watu kutoka Kusini mwa Asia.
Matumizi ya manjano yanaongezeka
Kashyap anasema kuwa manjano pia inatajwa katika maandishi ya takriban miaka 2,500 iliyopita.
Manjano inajulikana sana Kusini mwa Asia na kwa muda mrefu imeaminika kuwa na sifa za kuzuia maambukizi na kupunguza uvimbe.
Kashyap, anayeishi Dubai, anasema, "Ninapokuwa mgonjwa, kitu cha kwanza kinachonijia akilini ni manjano. Hunipa nafuu kubwa. Hutoa utulivu, husaidia kuponya, na pia huamsha kumbukumbu za zamani."
Nchini India, pia ni sehemu ya 'Sherehe ya Haldi', desturi ya kabla ya harusi ambapo mchanganyiko wa manjano hupakwa kama pambo la uso.
Mauzo sasa yanaongezeka kwa kasi huku watu wa nchi za Magharibi wakigundua faida za muda mrefu za manjano.
Virutubisho vya manjano, ambavyo kwa kawaida huwa na kiambato kinachoitwa curcumi, vinaaminika kuwa ndivyo vinavyotoa faida hizo za kiafya. Vinauzwa kwa madai ya kusaidia mambo mbalimbali, kuanzia kuboresha afya ya mifupa na viungo hadi kuimarisha kinga ya mwili.
Kashyap anasema kuwa mojawapo ya sababu za kuongezeka kwa umaarufu wa manjano ni mitandao ya kijamii, ambapo watu hushiriki uzoefu wao mzuri baada ya kutumia manjano.
Anasema, "Ikiwa mamilioni ya watu wanaamini kwa dhati kuwa manjano inaweza kutibu matatizo mengi, hilo hutuma ujumbe muhimu duniani kote.
Kisha, ikiwa ujumbe huo unaungwa mkono na kampeni za ushawishi pamoja na makampuni ya virutubisho, unakuwa na nguvu zaidi."
Je, muundo wa kikemia wa manjano ni mbaya?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, baadhi ya wataalamu wana mashaka kuhusu faida hizi za manjano. Dkt. Katherine Nelson, mtaalamu wa kemia kutoka Minnesota, Marekani, amechunguza zaidi ya machapisho 100 ya utafiti kuhusu *curcumin*.
Anasema, "Tuligundua kuwa ingawa kuna madai yanayotolewa kana kwamba inaweza kufaa kwa kila aina ya ugonjwa, kiuhalisia huenda haina matokeo makubwa."
Kulingana na Dkt. Nelson, tatizo la manjano huenda likawa katika muundo wake wa kikemia, jambo linalofanya iwe vigumu kuifanyia utafiti wa kisayansi.
Ina tabia ya kuitikia kwa nguvu kemikali nyingine na inaweza kuingilia kati majaribio ya utafiti, hii ina maana kwamba wakati mwingine inaweza kuonekana kama inafanya kazi kumbe sivyo.
Anaeleza kuwa mwili hauiingizi manjano vizuri mwilini. Inapoliwa, kiasi kidogo tu ndicho hufika kwenye mfumo wa damu. Hii ndiyo sababu watu wengi huichanganya na pilipili nyeusi ili kusaidia mwili kuinyonya vizuri zaidi.
"Kwa kweli, kutokana na muundo wake wa kikemia, ni moja ya vitu visivyofaa kabisa kutengenezewa dawa inayofanya kazi," anasema Dkt. Nelson.
Utafiti kuhusu manjano unasema nini?
Binzari ya manjano imefanyiwa utafiti wa kina kwa miongo kadhaa, lakini matokeo mara nyingi hutofautiana na ubora wa tafiti hizo hauko thabiti.
Profesa Amit Garg, bingwa wa magonjwa ya figo katika Kituo cha Sayansi ya Afya cha London huko Ontario, Canada, anasema kuwa tafiti nyingi zinazodai kuwepo kwa faida za manjano hazikufanywa kwa binadamu.
Yeye na wenzake walifanya tafiti mbili kati ya kubwa zaidi kuwahi kufanyika hadi sasa. Ya kwanza ililenga kubaini kama *curcumin* (kiambato kikuu cha manjano) inaweza kuzuia uharibifu wa figo na uvimbe kwa watu wanaofanyiwa upasuaji wa kurekebisha tatizo la kupanuka kwa aota (aortic aneurysm). Hata hivyo, jaribio hilo, lililohusisha wagonjwa 600, halikuonyesha faida yoyote.
Baadaye, walitumia *curcumin* katika mfumo wa chembechembe ndogo sana, kwa watu wenye ugonjwa wa figo ili kuona kama ingeboresha afya ya figo zao au kuzuia ugonjwa huo kuzidi kuwa mbaya.
Lakini wakati huu pia, hawakuweza kupata ushahidi wowote unaoweza kuthibitisha kuwa *curcumin* ina faida.
"Tulihisi kukatishwa tamaa kwa sababu tulipoanza jaribio hili, hatukudhani kuwa *curcumin* haifanyi kazi. Lengo letu halikuwa kuthibitisha kuwa haina ufanisi," anasema.
Lakini swali linajitokeza, ikiwa manjano Imekuwa yakitumika kama dawa au tiba kwa maelfu ya miaka, hasa nchini India, basi sababu ya matumizi hayo ni nini?
Dkt. Garg anasema kuwa kutenganisha kiambato mahususi kutoka kwenye kitu cha asili na kujaribu kutengeneza dawa kutokana nacho ni jambo tofauti kabisa na kula kitu hicho cha asili kwa ukamilifu wake au kukipaka kwenye ngozi.
Basi, je, wataalamu wanaona kuwa virutubisho vya gharama kubwa vina faida?
Profesa Garg anasema kuwa tatizo kubwa zaidi, mbali na gharama, ni kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa virutubisho hivi vinafanya kazi kweli. Anaeleza kuwa bidhaa za asili za afya hazikabiliwi na kanuni kali kama zile zinazotumika kwa dawa nyingine na bidhaa za kifamasia.
Anasema, "Nadhani tunapaswa kuwa na mtazamo wazi kuhusu hili, lakini lazima kuwe na kiwango fulani, ikiwa tunadai kuwa kitu kina faida mahususi, ni lazima dai hilo liungwe mkono na utafiti thabiti wa kisayansi wenye ubora wa juu."
Hata hivyo, haoni tatizo lolote katika kutumia manjano kwenye chakula.
Anasema, "Ikiwa watu wanapenda chakula chenye manjano, ningewashauri waendelee kukila."
How it works
Once you click Generate, Ollama reads this article and crafts 5 comprehension questions. Your answers are graded against the article content — general knowledge won't be enough. Score 70+ to count toward your certificate.
Questions are cached — you'll always get the same 5 for this article.