general4196 wordsRead on Arc Codex

Maafisa 8 wa meli ya kivita ya Marekani Abraham Lincoln watishia kujitoa uhai

Moja kwa moja, Maafisa 8 wa meli ya kivita ya Marekani Abraham Lincoln watishia kujitoa uhai USS Abraham Lincoln imekuwa ikifanya operesheni katika eneo la Mashariki ya Kati tangu Novemba mwaka jana na sasa iko njiani kurejea Marekani. Muhtasari - Joshua na Fury kukutana kwenye pambano la kihistoria - Saudi Arabia yafuta onyo la mashambulizi Jeddah na Makka - Upinzani Sudan Kusini wapinga uchaguzi wa Desemba - Israel yadai kumuua mkuu wa masuala ya fedha wa Hamas - Viza ya kiongozi wa kijeshi wa Sudan yakataliwa na Marekani, akitarajiwa kuhutubia mkutano wa UN - Rais Ruto ataka Afrika ipewe kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN - Trump atangaza dola billioni 2.45 za kujenga upya Gaza - BASATA yawachukulia hatua Harmonize, Nandy na waandaaji wa mashindano ya urembo - Wanajeshi 8 wa Marekani walijaribu kujiua ndani ya meli ya kivita ya USS Abraham - Iran yatoa onyo kali kwa majirani wanaotekeleza vikwazo vya kufunga anga zao - Tigray yakana kuanzisha mashambulizi, hofu ya kurejea kwa vita yazuka - Trump ampokea Xi Jinping Marekani huku mvutano kati ya mataifa hayo ukiendelea - Tetesi za soka Alhamisi: Barcelona yaondoa uwezekano wa kumsajili Alvarez - Iran yasema haitakubali kutishwa na Marekani, lakini iko tayari kwa mazungumzo Moja kwa moja Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi Maafisa 8 wa USS Abraham Lincoln watishia kujitoa uhai Maafisa wanane waliokuwa wakihudumu katika meli ya kivita ya USS Abraham Lincoln walijaribu kujitoa uhai wakati wa operesheni ya muda mrefu ya kijeshi ya Marekani Mashariki ya Kati, kwa mujibu wa kaimu Waziri wa Jeshi la Wanamaji la Marekani. Taarifa hiyo ilitolewa kupitia barua kwa Seneta wa New York, Kirsten Gillibrand, kujibu maswali kuhusu afya na ustawi wa wanamaji waliokuwa sehemu ya msafara huo. Familia za baadhi ya maafisa hao zimekuwa zikieleza wasiwasi kuhusu kuzorota kwa afya ya akili na mazingira magumu ya kazi wakati wa operesheni hiyo, ambayo ni sehemu ya shughuli za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran. USS Abraham Lincoln imekuwa ikifanya operesheni katika eneo hilo tangu Novemba mwaka jana na kwa sasa iko njiani kurejea Marekani. Katika barua hiyo, kaimu Waziri wa Jeshi la Wanamaji, Hong Kao, alisema makasisi watano wa kijeshi pamoja na wataalamu kadhaa wa afya ya akili walikuwa wametumwa ndani ya meli hiyo kusaidia mahitaji ya kiroho na kisaikolojia ya wanajeshi. BBC imewasiliana na Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa maoni zaidi kuhusu suala hilo. Alisema matukio hayo yalihusisha wafanyakazi wa USS Abraham Lincoln pamoja na wanamaji wa kikosi cha anga cha meli hiyo, wanajeshi wa kikosi kazi cha manowari za kivita pamoja na vikosi vyote vya anga vilivyokuwa vimepangiwa kuhudumu ndani ya meli. Soma pia: Xi awasili Marekani kwa mkutano na Trump: Tunachojua kufikia sasa Rais wa China, Xi Jinping, amewasili nchini Marekani kwa mkutano muhimu na Rais wa Marekani Donald Trump. Haya ndiyo mambo muhimu yatakayoangaziwa katika ziara ya Xi na mazungumzo yanayofanyika wiki hii: - Marekani na China zimefikia makubaliano ya kuongeza muda wa usitishaji wa vita vyao vya kibiashara, ambao ulitarajiwa kumalizika Novemba, hadi angalau Januari 10. - Xi na mkewe walipopokewa baada ya kushuka kutoka ndege yao, walipewa heshima ya zulia jekundu. Rais Trump na Mke wa Rais Melania Trump pia walikuwepo kuwakaribisha binafsi. - Katika taarifa iliyoandikwa, Xi amesema China na Marekani zinapaswa kuwa “washirika badala ya wapinzani”, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya serikali ya China. - Wakati Trump na Xi wakitafuta njia za kudhibiti uhusiano wao wenye changamoto, mmoja wao ameonyesha ukaribu na utayari mkubwa zaidi kuliko mwenzake, anaandika mwandishi wa BBC anayefuatilia China, Laura Bicker. - Ziara ya Xi pia inaweza kumuweka Trump katika hatari ya kukosolewa na baadhi ya wafuasi wake wa vuguvugu la MAGA, anaandika mwandishi wa BBC wa Ikulu ya Marekani, Bernd Debusmann Jr. - Xi ameandamana na baadhi ya viongozi wa juu zaidi katika serikali yake, akiwemo mshauri wake wa karibu Cai Qi na Waziri wa Mambo ya Nje Wang Yi. - Wakuu wa kampuni kubwa za teknolojia na akili bandia (AI) nchini Marekani wanatarajiwa kuhudhuria karamu ya kitaifa itakayowakutanisha viongozi hao wawili Alhamisi. - Bado haijabainika ikiwa viongozi wa sekta ya biashara ya China wamejumuishwa katika ujumbe wa Xi, kutokana na wasiwasi kwamba ushiriki wao unaweza kuchukuliwa na Beijing kama hatari ya kisiasa au kiuchumi. Kenya kuteketeza dawa za kulevya za thamani ya mabilioni ya fedha Mombasa Mamlaka za Kenya zinatarajiwa kuteketeza shehena ya dawa za kulevya aina ya methamphetamine yenye thamani ya Sh8.2 bilioni sawa na ($63M) mjini Mombasa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini humo. Maafisa wakuu wa usalama, wakiongozwa na Waziri wa Mambo ya Ndani Kipchumba Murkomen, wanatarajiwa kushuhudia zoezi hilo Alhamisi, huku serikali ikisema hatua hiyo inalenga kutoa ujumbe mkali kwa magenge ya usafirishaji wa dawa za kulevya katika ukanda wa Afrika Mashariki. Dawa hizo zilinaswa katika Bahari ya Hindi na zinahusishwa na kesi inayowakabili raia sita wa Iran wanaotuhumiwa kusafirisha zaidi ya tani moja ya methamphetamine. Mahakama ya Shanzu ilifahamishwa kuwa uteketezaji wa shehena hiyo ni njia salama zaidi ya kuhifadhi ushahidi huku kesi ikiendelea kusikilizwa. Watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kusafirisha kilogramu 1,036 za methamphetamine ye thamani ya takriban dola milioni 63 za Kimarekani. Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa Mahakama ya Shanzu kuwa upande wa mashtaka umewasilisha ushahidi wa kutosha kuwafanya watuhumiwa hao wajibu tuhuma zinazowakabili, baada ya mashahidi 12 kutoa ushahidi wao mahakamani. Joshua na Fury kukutana kwenye pambano la kihistoria Mabondia wa uzani wa juu wa Uingereza, Anthony Joshua na Tyson Fury, wanatarajiwa kukutana katika pambano lao lililosubiriwa kwa muda mrefu tarehe 11 Desemba kwenye Uwanja wa Principality mjini Cardiff. Pambano hilo, ambalo limekuwa likisubiriwa kwa zaidi ya muongo mmoja, litapeperushwa moja kwa moja kupitia Netflix, huku waandaaji wakidokeza litacheleweshwa kuanza ili kuwafikia watazamaji wa Marekani. Joshua na Fury wanatarajiwa kukutana ana kwa ana katika mkutano wa waandishi wa habari jijini London Septemba 30, kuashiria mwanzo wa maandalizi ya moja ya mapambano makubwa zaidi katika historia ya masumbwi ya Uingereza. Pigano hilo linaandaliwa kwa ushirikiano kati ya kampuni ya The Ring, inayoungwa mkono na mfadhili wa masumbwi wa Saudi Arabia Turki Alalshikh, na Zuffa Boxing chini ya rais wa UFC, Dana White. Maelezo zaidi: Saudi Arabia yafuta onyo la mashambulizi Jeddah na Makka Mamlaka ya Ulinzi wa Raia nchini Saudi Arabia ilitoa onyo la tahadhari kuhusu hatari inayoweza kutokea katika maeneo kadhaa, yakiwemo mji mtakatifu wa Mecca, eneo la Tabuk kaskazini-magharibi, maeneo ya pwani ya Bahari ya Shamu yanayojumuisha Jeddah na Yanbu, pamoja na mji wa Taif. Hata hivyo, dakika chache baadaye, mamlaka hiyo ilitangaza kuwa tishio lililoripotiwa katika maeneo hayo limeondolewa na kufuta onyo hilo. Onyo hilo lilikuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka kati ya Saudi Arabia na waasi wa Houthi nchini Yemen. Katika wiki za hivi karibuni, maeneo mbalimbali ya Saudi Arabia yameripotiwa kukumbwa na mashambulizi yanayohusishwa na Wahouthi, hali inayozidisha wasiwasi wa kiusalama nchini humo. Soma pia: Upinzani Sudan Kusini wapinga uchaguzi wa Desemba Chama kikuu cha upinzani nchini Sudan Kusini, SPLM-IO, kimetangaza kuwa hakitashiriki katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huu, kikidai kuwa mazingira yanayohitajika kwa uchaguzi huru, wa haki na wa kuaminika bado hayajatekelezwa. Hatua hiyo imekuja wakati chama hicho, kwa kushirikiana na makundi mengine ya upinzani na asasi za kiraia, kikiziandikia IGAD, Umoja wa Afrika na wadhamini wengine wa mkataba wa amani wa mwaka 2018, kikionya kuhusu kile kilichokitaja kuwa mgogoro wa kikatiba na uhalali wa uongozi nchini humo. Katika barua yao, makundi hayo yamedai kuwa utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 umekwama, yakitaja kushindwa kutekelezwa kwa vipengele muhimu vya mkataba huo pamoja na hatua za upande mmoja zilizochukuliwa na serikali ya Rais Salva Kiir. Upinzani umesema hautashiriki wala kuhalalisha uchaguzi wowote utakaofanyika bila mageuzi muhimu ya kikatiba, kisiasa na kiusalama, ukisisitiza kuwa masharti ya msingi ya uchaguzi wa haki bado hayajatimizwa. Makundi hayo sasa yanaitaka IGAD, Umoja wa Afrika na washirika wa kimataifa kuongoza mazungumzo ya kitaifa yatakayowezesha kupatikana kwa mwafaka mpya wa kikatiba nchini humo. Kaimu mwenyekiti wa SPLM-IO, Nathaniel Oyet, amesema baadhi ya maeneo ya Sudan Kusini bado yako chini ya udhibiti wa upinzani, jambo ambalo linaibua maswali kuhusu uwezo wa wananchi wa maeneo hayo kushiriki uchaguzi. Msimamo wa upinzani umeibuka siku chache baada ya Rais Salva Kiir kuivunja serikali ya mpito na bunge, pamoja na kusaini marekebisho ya sheria ya uchaguzi yaliyoondoa masharti ya kuwepo kwa katiba ya kudumu na sensa ya kitaifa kabla ya uchaguzi. Wakati serikali ikieleza kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuwezesha uchaguzi wa Desemba 22 kufanyika kwa wakati, viongozi wa upinzani wanadai ni hatua zinazolenga kuimarisha mamlaka ya Rais Kiir kabla na baada ya uchaguzi huo. Soma pia: Israel yadai kumuua mkuu wa fedha wa Hamas Khan Yunis Jeshi la Ulinzi la Israel IDF, linadai kuwa limemuua Mohammed Abu Alwan, ambaye limemtaja kuwa mkuu wa masuala ya fedha wa Hamas, katika shambulio la Jumatano mjini Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. Katika taarifa, IDF hilo limesema Abu Alwan alikuwa na jukumu la kusimamia na kuamua bajeti za matawi yote ya Hamas, pamoja na kusimamia mtiririko wa fedha za kundi hilo. Israel imeeleza kuwa chini ya usimamizi wake, takriban dola milioni 330 za Kimarekani, zilitumika kufadhili shughuli za Hamas. Kwa mujibu wa jeshi la Israel, Abu Alwan alikuwa miongoni mwa viongozi muhimu waliosaidia kudumisha uwezo wa kifedha, mamlaka na shughuli za Hamas katika Ukanda wa Gaza. Soma zaidi: Viza ya kiongozi wa kijeshi wa Sudan yakataliwa na Marekani, akitarajiwa kuhutubia mkutano wa UN Marekani imezuia viza ya mkuu wa jeshi la Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, kabla ya ziara yake iliyopangwa ya Umoja wa Mataifa (UN), katika hatua ambayo vyanzo vya Sudan na vingine vinasema inahusishwa na pendekezo la kusitisha mapigano linaloungwa mkono na Marekani ambalo Khartoum imekataa. Kulingana na shirika la habari la Reuters, hatua hiyo inatishia kuongeza mvutano kati ya Washington na jeshi la Sudan wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe vinaendelea, vita ambavyo Umoja wa Mataifa unavitaja kuwa miongoni mwa migogoro mikubwa zaidi ya kibinadamu duniani. Chanzo kimoja cha ngazi ya juu nchini Sudan kimesema Burhan ameahirisha safari yake kwenda New York, lakini bado hajapokea taarifa rasmi kwamba viza yake imekataliwa. “Serikali ya Sudan inaelezea masikitiko yake makubwa, kwa sababu hii ni ukiukaji wa Mkataba wa UN na sheria za kimataifa,serikali ya Sudan iko tayari kwa amani” chanzo hicho kilisema Balozi wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, amemwomba Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, kuingilia kati, akisema kupitia barua kwamba kumzuia Burhan kuhudhuria mkutano mkuu wa UN kutakiuka wajibu wa Umoja wa Mataifa kwa nchi wanachama. Kwa mujibu wa chanzo cha kidiplomasia cha Sudan ameiambia Reuters kuwa, maafisa wa Marekani wameweka sharti la Burhan kuhudhuria mkutano huo, ni lazima akubali kusitisha mapigano kwa siku 90, kama ilivyopendekezwa na Mshauri Mkuu wa Marekani anayehusika na Masuala ya Waarabu na Afrika, Massad Boulos. Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikataa kutoa maoni kuhusu viza ya Burhan. Msemaji wa Wizara hiyo, Tommy Pigott, alisema katika taarifa baadaye kuwa Jeshi la Sudan (SAF), kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF), na viongozi wao “hawawakilishi utawala halali wa kikatiba nchini Sudan.” “Serikali ya Marekani na Rais Trump wako tayari kufanya kazi na yeyote aliye mshirika wa dhati katika juhudi za kuleta amani nchini Sudan.” Mvutano huo unaashiria kudorora kwa uhusiano kati ya sudan na Marekani, tangu kuzuka kwa vita nchini humo mwezi Aprili 2023. Burhan alikuwa anatarajiwa kuhutubia Mkutano Mkuu wa UN hii leo, ila hotuba hiyo itatolewa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Sudan, Mohieldin Salem. Soma pia: Rais Ruto ataka Afrika ipewe kiti cha kudumu katika Baraza la Usalama la UN Rais wa Kenya William Ruto ametoa wito wa mageuzi kufanyika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuipa Afrika uwakilishi wa haki na wa kudumu katika maamuzi yanayohusu amani na usalama duniani. Akizungumza wakati wa Mjadala Mkuu wa Kikao cha 81 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Ruto alisema UN imetoa mchango mkubwa katika kukuza amani, utawala na maendeleo, lakini pia imeshindwa kutimiza kikamilifu ahadi zake. Alisema migogoro bado inaendelea, huku sheria za kimataifa zikitumiwa kwa viwango tofauti na ukosefu wa usawa ukiendelea kuwepo katika taasisi za kimataifa. Rais Ruto anataka Afrika ipewe uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la UN, ikiambatana na haki na mamlaka zote zinazotolewa kwa wanachama wa kudumu. “Afrika lazima iwe na sauti yenye nguvu katika maamuzi yanayounda amani na usalama duniani.” Ruto pia ametaka mageuzi kufanyika katika mfumo wa kimataifa wa kifedha, akisema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na gharama kubwa za kupata fedha za maendeleo, na wao huenda kutumia rasilimali ambazo zingeelekezwa katika huduma muhimu kulipa madeni. Rais huyo aliongezea kuwa nchi zinazoendelea zinahitaji upatikanaji mikopo nafuu ya muda mrefu, ili kufadhili miradi ya maendeleo. Trump atangaza dola billioni 2.45 za kujenga upya Gaza Bodi ya amani inayoongozwa na Rais wa Marekani Donald Trump, imetangaza mpango wa dola bilioni 2.45, itakayotumika kuanza mchakato wa kujenga upya eneo la Gaza. Tangazo hilo limetolewa pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa. Kwa mujibu wa mpango huo, bajeti hiyo itatumika kwa kipindi cha miezi sitana kutekeleza miradi 66. Miongoni mwa maeneo muhimu ni ujenzi wa makazi, uzalishaji wa umeme kwa kutumia jenereta za dizeli, pamoja na ukusanyaji wa taka na vifusi. Hata hivyo, timu ya amani imesema fedha zaidi zinahitajika ili kutekeleza mpango huo. Hadi sasa, nchi na wafadhili kadhaa wameahidi kutoa dola bilioni 18, lakini ni dola milioni 280 pekee ambazo zimepatikana kwa ajili ya mpango huo. Timu hiyo inakadiria kuwa takribani dola bilioni 71.4 zitahitajika katika kipindi cha miaka 10 ijayo ili kujenga upya na kurekebisha Gaza kikamilifu. Jared Kushner, mkwe wa Donald Trump na mwanachama wa Bodi ya Utendaji ya Gaza katika Tume ya Amani, alikiri kuwa mradi huo umekabiliwa na “ucheleweshaji mbalimbali katika maeneo tofauti.” Soma pia: BASATA yawachukulia hatua Harmonize, Nandy na waandaaji wa mashindano ya urembo Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemtaka msanii Rajab Abdul Kahali, maarufu kama Harmonize, kuchukua hatua za kurekebisha ukiukwaji wa maadili baada ya kutuhumiwa kusambaza video ya wimbo wake “Kudos”, ambayo kwa mujibu wa Baraza hilo inakiuka maadili ya Mtanzania na heshima ya wasikilizaji na watazamaji. Kwa mujibu wa BASATA, Harmonize hakuwasilisha utetezi wala maelezo ya ziada kabla ya uamuzi kutolewa. Baraza hilo limemuamuru kuiondoa video hiyo kwenye mitandao yake ya kijamii, kulipa faini ya shilingi milioni tano ndani ya siku 14 na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza masharti hayo. BASATA pia imemchukulia hatua mkurugenzi wa video hiyo, Kennedy David Sanga, baada ya kubaini kuwa alikiuka maadili ya sanaa kwa kuiongoza video hiyo. Ameamriwa kuiondoa video hiyo, kulipa faini ya shilingi milioni tano ndani ya siku 14 na kusitisha shughuli za sanaa hadi atakapotekeleza masharti hayo. Wakati huo huo, msanii Faustina Charles Mfinanga, maarufu kama Nandy, amepigwa faini shilingi milioni tatu za Tanzania baada ya kukiri kosa la kuvaa mavazi yasiyo na staha alipokuwa akitumbuiza katika fainali ya Miss Universe Tanzania 2026. BASATA imesema Nandy tayari ameiondoa video hiyo na kulipa faini hiyo, hivyo ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za sanaa chini ya uangalizi wa Baraza hilo. BASATA pia imewatoza faini waandaaji wa mashindano mawili ya urembo. Avil Contractors Company Ltd, waandaaji wa Miss Grand Tanzania, wametozwa faini ya shilingi milioni tatu kwa kuendesha shindano hilo bila kibali cha tukio kutoka BASATA. Kwa upande wa Millen Privé & Co. Lifestyle Limited, waandaaji wa Miss Universe Tanzania, wametozwa faini ya shilingi milioni tatu za Tanzania na kupewa onyo kali. Wanajeshi 8 wa Marekani walijaribu kujiua ndani ya meli ya kivita ya USS Abraham Kaimu Katibu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, Hong Kao, amefichua kuwa wanajeshi wanane waliokuwa kwenye meli ya kubeba ndege ya USS Abraham Lincoln walijaribu kujiua wakati wa safari ya muda mrefu ya kikazi. Kauli hiyo ilitolewa Jumanne kupitia barua aliyomwandikia Seneta Kirsten Gillibrand wa New York, ambaye alikuwa ameibua maswali kuhusu hali na ustawi wa wanajeshi waliokuwa kwenye meli hiyo. Familia za wanajeshi hao tayari zilikuwa zimeeleza wasiwasi kuhusu afya ya akili ya wanamaji, ambao walikuwa wakikabiliwa na misheni ndefu, mazingira magumu na msongo wa mawazo. Meli ya Abraham Lincoln ilikuwa imepelekwa katika misheni tangu Novemba mwaka jana na ilikuwa Mashariki ya Kati katika operesheni za kijeshi za Marekani dhidi ya Iran. Kwa sasa, meli hiyo iko njiani kurejea Marekani. Katika barua hiyo, Kao alisema kulikuwa na makasisi watano wa kijeshi pamoja na wataalamu kadhaa wa afya ya akili waliokuwa ndani ya meli hiyo ili kushughulikia mahitaji ya kiroho na kisaikolojia ya wanajeshi. Kwa mujibu wake, watu hao wanane waliojaribu kujiua hawakuwa tu wafanyakazi wa Abraham Lincoln, bali pia walitoka katika kikosi cha anga, kikundi cha mashambulizi, waharibifu wa majini na vitengo vingine vya usaidizi. Ingawa Jeshi la Wanamaji la Marekani limewahi kukiri kuwepo kwa changamoto za kiutendaji, limepuuza dhana kwamba kulikuwa na mzozo mkubwa wa afya ya akili ndani ya meli hiyo iliyokuwa na takribani wanajeshi 5,000. Kao pia alisema taarifa kuhusu mifumo ya mabomba iliyoharibika na uhaba mkubwa wa chakula kipya zilitiwa chumvi. Hata hivyo, alikiri kuwepo kwa hitilafu za mabomba katika baadhi ya maeneo, matatizo katika mitambo ya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari na upungufu wa chaguo la vyakula kwa kipindi fulani. Kwa upande wake, Seneta Gillibrand aliikosoa serikali ya Trump kwa namna ilivyoshughulikia malalamiko hayo hapo awali, akisema kuwa kuwahudumia wanajeshi kwa namna hiyo ni “jambo lisilokubalika kabisa.” Kwa mujibu wake, matatizo yaliyokuwa yakitajwa kuwa ni “habari za uongo” kwa kweli yalikuwa hali nzito iliyokuwa ikiendelea kuwa mbaya kwa wanajeshi. Abraham Lincoln iliondoka California Novemba mwaka jana. Misheni yake ilipangwa kumalizika mwezi Mei, lakini ikaongezwa mara kadhaa. Mwezi Agosti, USS George Washington ilitumwa Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya Abraham Lincoln, ambayo ilikuwa imemaliza misheni ya miezi tisa. Kwa mujibu wa takwimu, kujitoa uhai ni miongoni mwa sababu kuu za vifo katika Jeshi la Wanamaji na Jeshi la Wanamaji la Marekani. Utafiti uliochapishwa Januari 2025 na kuwahusisha wanajeshi 956 wa majini ulibaini kuwa wanajeshi wanaohudumu kwenye meli wako katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na msongo mkali wa kisaikolojia ikilinganishwa na wanajeshi wa matawi mengine ya jeshi la Marekani. Utafiti huo unaonyesha kuwa mazingira duni ya kuishi, kelele za mara kwa mara, ratiba ngumu za kazi na ukosefu wa muda wa kutosha wa kupumzika na kulala ni miongoni mwa mambo yanayoweza kuathiri vibaya afya ya akili. Soma zaidi: Iran yatoa onyo kali kwa majirani wanaotekeleza vikwazo vya kufunga anga zao Mohsen Rezaei, katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amezionya nchi jirani na Iran katika mahojiano na televisheni ya Iran kwamba “iwapo zitaungana na vikwazo vya Marekani dhidi ya safari za anga, viwanja vyao vya ndege pia havitaweza kuendesha safari za ndege.” “Hamuwezi kuzuia safari za wafanyabiashara wetu, ndege zetu zishindwe kufanya safari na bidhaa zetu zishindwe kuingia kupitia anga, halafu ninyi mkashirikiana na Marekani na sisi tuangalie tu?” alisema. Vikwazo vya Marekani dhidi ya mashirika ya ndege ya Iran vimeanza kutekelezwa leo. Safari nyingi za ndege za Iran kwenda nchi mbalimbali zimesitishwa, ingawa baadhi ya nchi bado zinaruhusu mashirika ya ndege ya Iran kutumia viwanja vyao vya ndege. Mohsen Rezaei pia amesema taarifa kuhusu mazungumzo na ujumbe mbalimbali pembezoni mwa mkutano wa Umoja wa Mataifa “si mazungumzo, bali ni uwasilishaji tu wa masharti.” Amesema hakuna masharti mapya yaliyoongezwa wala yaliyopunguzwa, na kwamba Mlango-Bahari wa Hormuz hautafunguliwa hadi masharti hayo yatakapoondolewa. Rezaei amesisitiza kuwa Iran “imewasilisha masharti saba, si matatu.” Amesema maafisa wa Iran walikubaliana kuhusu hilo kwa siku mbili au tatu, na wakaafikiana kuwa watawaeleza wapatanishi masharti ya Iran. Soma pia: Tigray yakana kuanzisha mashambulizi, hofu ya kurejea kwa vita yazuka Ubalozi wa Marekani nchini Ethiopia umeituhumu TPLF kwa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi. Katika taarifa iliyotolewa, Septemba 23, 2026, Balozi wa Marekani nchini Ethiopia, Ervin J. Massinga, alisema amesikitishwa kuona uongozi wa TPLF, ambao Marekani iliwekea vikwazo mapema mwaka huu, ukifanya “uamuzi usio sahihi wa kuanzisha mashambulizi makubwa.” Hata hivyo, uongozi wa eneo la Tigray umekanusha vikali tuhuma hizo. Makamu wa rais wa eneo hilo, Amanuel Assefa, alielezea kauli ya balozi huyo katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii kuwa “ya kukatisha tamaa sana,” huku akiishutumu Marekani na wajumbe wa Umoja wa Afrika kwa kupuuza athari za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara ya anga yanayofanywa na kile alichokiita “utawala wa kidikteta.” Amesema mashambulizi ya mabomu yamesababisha “vifo vingi vya raia” huko Tigray, akieleza hali ngumu wanayokabili mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao na wanaoishi katika kambi za muda. “Ni vigumu kuelewa jinsi kuhamishia lawama upande mwingine kwa namna hii kunavyoweza kuchukuliwa kuwa ni haki,” Amanuel aliandika, akiongeza kuwa wasiwasi kuhusu kutokuegemea upande wowote katika diplomasia bado ni “jambo la kutia wasiwasi mkubwa.” Serikali ya Ethiopia na chama tawala katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo zimeshutumiana kuhusika na mashambulizi hayo, hali inayozua hofu ya kurejea kwa mapigano makubwa. Getachew Reda, waziri wa serikali na mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, amesema wapiganaji wa Tigray wamechukua udhibiti wa viwanja vya ndege vinavyodhibitiwa na serikali ya shirikisho huko Tigray, na wameanzisha mashambulizi katika maeneo jirani ya Afar na Amhara. Awali, mamlaka za Tigray zilisema vikosi vyao vimelazimika kuingia katika “vita vya kujihami.” Kauli hiyo ilitolewa baada ya kuripotiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Tigray. Vita vya miaka miwili huko Tigray vilimalizika mwaka 2022, lakini katika miezi ya hivi karibuni pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kukiuka makubaliano ya amani. Vita hivyo vilikuwa miongoni mwa migogoro iliyosababisha vifo vingi zaidi katika karne hii. Mpatanishi wa Umoja wa Afrika alikadiria kuwa karibu watu 600,000 walifariki katika mzozo huo, uliosababisha eneo hilo kuingia katika hali mbaya ya kibinadamu inayokaribia kuwa janga la njaa. Soma Pia: Trump ampokea Xi Jinping Marekani huku mvutano kati ya mataifa hayo ukiendelea Rais wa Marekani Donald Trump amempokea Rais wa China Xi Jinping nchini Marekani kwa ziara ya siku tatu, huku viongozi hao wakitarajiwa kujadili masuala nyeti yanayoendelea kuathiri uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye uchumi mkubwa duniani. Xi amewasili Washington katika ziara yake ya kwanza nchini Marekani baada ya takriban miaka mitatu. Trump amempokea Xi katika kituo cha kijeshi cha Joint Base Andrews, Maryland, katika hafla yenye heshima za kijeshi, ikiwemo muziki wa bendi ya kijeshi, mizinga na ndege ya kivita ya B1 iliyopita angani. Mazungumzo yao yanatarajiwa kugusa biashara, teknolojia, Taiwan na mzozo wa Iran, huku Washington na Beijing zikiwa bado zinakabiliwa na tofauti kubwa katika maeneo hayo. Wakati huo huo, Waziri wa Hazina wa Marekani Scott Bessent amesema Marekani na China zimekubaliana kuongeza muda wa makubaliano yao ya kusitisha vita vya kibiashara hadi Januari. Hata hivyo, matarajio ya kufikiwa kwa makubaliano makubwa zaidi katika ziara hiyo yanaonekana kuwa madogo, huku suala la Taiwan likiwa miongoni mwa mada ambazo Beijing inatarajiwa kulisisitiza. Kwa upande wake, Xi amesema Marekani na China zinapaswa kuwa washirika badala ya wapinzani, wakati viongozi hao wakijaribu kudhibiti tofauti zao katika biashara, teknolojia na masuala ya kimkakati. Ziara hiyo inafanyika wakati uhusiano kati ya Washington na Beijing ukiendelea kuwa muhimu kwa uchumi wa dunia, huku maamuzi ya viongozi hao yakitarajiwa kuwa na athari zaidi ya mataifa hayo mawili. Soma Pia: Tetesi za soka Alhamisi: Barcelona yaondoa uwezekano wa kumsajili Alvarez Barcelona imeondoa uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa Argentina, Julian Alvarez, kutoka Atletico Madrid katika dirisha la usajili la Januari. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 anasubiri kuona iwapo Paris St-Germain au Arsenal itawasilisha ofa ya kumsajili, au kama ataamua kubaki Atletico Madrid.(Fichajes - in Spanish) Liverpool haiko tayari kumuuza kiungo wa Ujerumani, Florian Wirtz, mwenye umri wa miaka 23, kwenda Bayern Munich katika dirisha la usajili la Januari. Hata hivyo, mabingwa hao wa Ujerumani wanaweza kujaribu kumsajili msimu ujao wa kiangazi iwapo winga wa Ufaransa, Michael Olise, mwenye miaka 24, atakataa kusaini mkataba mpya. (Christian Falk - Bayern Insider/Bild) Chelsea imewaweka kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye miaka 23, pamoja na kiungo wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Adam Wharton, mwenye miaka 22, kama walengwa wake wakuu katika eneo la kiungo. Klabu hiyo ya London Magharibi haionyeshi tena nia ya kumsajili kiungo wa Monaco na Senegal, Lamine Camara, mwenye miaka 22.(CaughtOffside, external) Aston Villa inataka kumpa kiungo wa Argentina, Emi Buendia, mwenye miaka 29, mkataba mpya kama zawadi kwa kiwango bora alichoonyesha hivi karibuni. (Mail) Beki wa kushoto wa England, Luke Shaw, mwenye miaka 31, anaweza kuondoka Manchester United baada ya mkataba wake wa sasa kumalizika mwishoni mwa msimu ujao. (Teamtalk) Udinese inatarajiwa kumsajili beki wa Austria, David Alaba, mwenye miaka 34, ambaye aliondoka Real Madrid msimu huu wa kiangazi. (Fabrizio Romano) Pia unaweza kusoma: Iran yasema haitakubali kutishwa na Marekani, lakini iko tayari kwa mazungumzo Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amesema kuwa Iran haitawahi “kupiga magoti” baada ya karibu miezi saba ya vita dhidi ya Marekani na Israel, huku akisisitiza kuwa Tehran iko tayari kufikia suluhisho la kidiplomasia la mzozo huo. Akijibu tishio la Rais wa Marekani Donald Trump kwamba Jamhuri ya Kiislamu inaweza “kuangamizwa kabisa” iwapo makubaliano hayatapatikana hivi karibuni, Pezeshkian aliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa: “Upinzani wa wananchi wa Iran utaongezeka zaidi mbele ya vikwazo, kuongezwa kwa shinikizo na vitisho.” Pezeshkian pia alisisitiza kuwa makubaliano yoyote lazima yajumuishe kusitishwa kwa kile Iran inachokitaja kuwa ni kizuizi cha Marekani kinachozuia meli za Iran kutumia njia muhimu ya majini katika Ghuba. “Haikubaliki kwamba kila mtu anufaike na Mlango-Bahari wa Hormuz huku sisi tukinyimwa fursa ya kuutumia,” alisema. Hakukuwa na tamko la haraka kutoka upande wa Marekani, ambao ujumbe wake ulitoka katika ukumbi wa Baraza Kuu mwanzoni mwa hotuba ya Pezeshkian. Soma Zaidi: Hujambo na karibu kwa matangazo yetu ya moja kwa moja ya 24/09/2026.

How it works

Once you click Generate, Ollama reads this article and crafts 5 comprehension questions. Your answers are graded against the article content — general knowledge won't be enough. Score 70+ to count toward your certificate.

Questions are cached — you'll always get the same 5 for this article.