general2935 wordsRead on Arc Codex

Mzozo wa Iran: IRGC yadai kushambulia kambi za jeshi la Marekani nchini Kuwait

Mzozo wa Iran: IRGC yadai kushambulia kambi za jeshi la Marekani nchini Kuwait Vikosi vya Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislam nchini Iran (IRGC) vinasema kuwa vimechoma moto na kuharibu majengo mawili ya kuhifadhia ndege zisizo na rubani pamoja na tangi la mafuta kwa ajili ya ndege za kijeshi na helikopta katika shambulio dhidi ya kambi ya anga ya Ali al-Salem nchini Kuwait Alhamisi asubuhi. Madai hayo bado halijathibitishwa na maafisa wa Kuwait na Marekani. Idara ya uhusiano wa umma ya IRGC ilielezea shambulio hilo kuwa sehemu ya "Operesheni Nasr 2" na hatua ya kujibu uwepo wa vikosi vya Marekani katika eneo hilo, lakini haikutoa maelezo kuhusu aina ya silaha zilizotumika, ukubwa wa uharibifu, au uwezekano wa kuwepo kwa majeruhi au vifo. Awali, IRGC ilidai kushambulia kambi ya Ali al-Salem—ambayo iko kaskazini-magharibi mwa Kuwait na hutumiwa na vikosi vya Marekani—na kusababisha uharibifu mkubwa kwa miundombinu na vikosi vya Marekani. Madai hayo hayakuthibitishwa na Marekani au Kuwait wakati huo. Kambi ya Ali al-Salem iko kaskazini-magharibi mwa Kuwait na hutumiwa na vikosi vya Marekani. China yakanusha madai ya kuuzia Iran mifumo ya ulinzi Wizara ya Ulinzi ya China imekanusha ripoti kuhusu mpango wake wa kuipatia Iran mamia ya mifumo ya ulinzi wa anga na kuzitaja kuwa "za uongo na zisizo na msingi wowote." Alipoulizwa kuhusu taarifa hiyo siku ya Alhamisi, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya China, Jiang Bin, alisema madai hayo si ya kweli. Awali, Wizara ya Mambo ya Nje ya China ilikuwa imesema taarifa hiyo kuhusu makubaliano hayo haina msingi wowote. Iran inatarajiwa kupokea jumla ya mifumo kati ya 300 na 400 ya ulinzi wa anga inayoweza kubebwa na mtu mmoja na kutengenezwa nchini China katika kipindi cha wiki chache zijazo; hayo yaliripotiwa na shirika la habari la Reuters siku ya Jumatano, likinukuu vyanzo vitatu vyenye taarifa kuhusu suala hilo. Vyanzo hivyo vilisema kuwa makubaliano hayo yanahusisha makombora ya aina ya QW-12 na FN-16, na thamani yake inakadiriwa kuwa kati ya dola milioni 60 na milioni 70. Inaripotiwa kuwa mkataba huo ulitiwa saini na kampuni yenye makao yake Hong Kong, ambayo inasemekana ilifanya kazi kama mpatanishi kati ya Iran na msambazaji wa China. Vyanzo vya Reuters vilisema kuwa shehena za awali zilipaswa kusafirishwa kutoka mji wa Urumqi ulioko magharibi mwa China na kupelekwa Iran kupitia Pakistan. Jeshi la Pakistan limekanusha kuhusika na uwezekano wa uhamishaji wa mifumo hiyo, likiita sehemu hiyo ya ripoti kuwa "ya kubuni na isiyo sahihi." Vyanzo vya Reuters pia vilisema kuwa licha ya kutiwa saini kwa mkataba huo, muda wa kuwasilisha mzigo, idadi ya mifumo na maelezo mengine ya utekelezaji wake yanaweza kubadilika. Shule ya wasichana ya Oprah Winfrey kufungwa Afrika Kusini Baada ya karibu miongo miwili ya kuwahudumia wasichana kutoka mazingira duni nchini Afrika Kusini, shule iliyoanzishwa na mwana harakati maarufu Oprah Winfrey inatarajiwa kufungwa mwaka ujao. Tangazo hilo limezua mjadala mkubwa mtandaoni. Oprah Winfrey amesema shule hiyo itakabidhiwa kwa Idara ya Elimu ya Mkoa wa Gauteng, kama ilivyokuwa katika makubaliano ya awali wakati shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007. Shule hiyo, inayojulikana kwa jina la Oprah Winfrey Leadership Academy for Girls, ilianzishwa baada ya mazungumzo kati ya Oprah na aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Dhamira ilikuwa kuwapa wasichana wenye vipaji kutoka familia zisizojiweza fursa ya kupata elimu bora. Wanafunzi wa shule hiyo walipata ufadhili katika shule ya bweni iliyokuwa na vifaa vya kisasa. Wakati ilipofunguliwa shule hiyo ilivutia hisia za wengi kwa kuwa na majengo ya kifahari, ikiwa ni pamoja na kumbi za maonyesho, maeneo maalum ya kufanya mazoezi ya aina mbali mbali na hata saluni ya urembo. Hata hivyo sasa Oprah anasema anataka kufikia wasichana wengi zaidi. Badala ya kuendesha shule moja, taasisi hiyo itabadilishwa kuwa mpango wa ufadhili wa masomo utakaowezesha wanafunzi wenye sifa kujiunga na shule bora mbalimbali nchini humo. Wanafunzi ambao bado watakuwa wakisoma shuleni humo wakati shule itakapofungwa pia watahamishiwa katika shule nyingine kwa ufadhili kamili wa masomo. Lakini historia ya shule hiyo haijakosa changamoto.Baadhi ya wakosoaji waliwahi kuhoji gharama kubwa zilizotumika kujenga shule hiyo ya kifahari, wakisema fedha hizo zingesaidia wanafunzi wengi zaidi kama zingewekezwa katika maeneo mengine ya nchi.Muda mfupi baada ya shule kufunguliwa, madai ya unyanyasaji dhidi ya mwanafunzi yaliibuka yakimhusisha mmoja wa wafanyakazi wa zamani. Kesi hiyo baadaye ilifikishwa mahakamani lakini mtuhumiwa aliachiliwa huru. Na mwaka 2011, kulikuwa na taarifa zilizoibua mjadala mkubwa baada ya mwanafunzi mmoja kulazwa hospitalini katika mazingira yaliyohusishwa na kifo cha mtoto mchanga. Uchunguzi ulifunguliwa, lakini matokeo yake hayakuwekwa wazi kwa umma. Kwa sasa haijulikani shule hiyo itatumika kwa shughuli gani baada ya kukabidhiwa kwa serikali ya mkoa. Hata hivyo, Idara ya Elimu ya Gauteng imesema itaendelea kulinda na kuendeleza urithi wa taasisi hiyo. Jeshi la Sudan latuhumiwa kuwaua raia 24 katika shambulio la droni Takribani watu 24, wengi wao wanawake na watoto, wanaripotiwa kuuawa katika shambulio la ndege isiyo na rubani katika kijiji cha Sharshar katika eneo la West Bara, jimbo la Kordofan Kaskazini, kulingana na shirika la kutetea haki za binadamu la Darfur Victims Advocacy. Shirika hilo liliwanukuu mashuhuda walioeleza kuwa ndege isiyo na rubani inayohusishwa na Jeshi la Sudan (SAF) ilifanya shambulio hilo mnamo tarehe 29 Julai, ikilenga eneo la Sharshar mwendo wa saa saba unusu kwa saa za Sudan. Kundi hilo lilisema linawajibisha jeshi kikamilifu kwa uhalifu huo. Muungano wa Sudan Founding Alliance, ambao ni muungano wa kisiasa na kijeshi unaoungwa mkono na kundi la wanamgambo la Rapid Support Forces (RSF), pia lililituhumu jeshi kwa kufanya shambulio hilo, likisema kuwa nyumba za raia na miundombinu zililengwa. Jeshi la Sudan (SAF) halijatoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo. BBC haijathibitisha madai yaliyotolewa kuhusu shambulio hilo. Shambulio hilo liliripotiwa siku chache baada ya jeshi na vikosi washirika kutangaza kulomboa mji muhimu wa kimkakati wa Bara kutoka mikononi mwa RSF. Mji huo, ulioko Kordofan Kaskazini, ni muhimu kutokana na eneo lake katika njia zinazounganisha Sudan ya Kati na eneo la Darfur. Udhibiti wa Kordofan Kaskazini umekuwa eneo muhimu katika vita vya Sudan, huku pande zote mbili, SAF na RSF, zikigombea ushawishi katika eneo hilo linalounganisha maeneo muhimu. Guterres ana wasiwasi baada ya mapigano kuzuka tena kati ya Marekani na Iran Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amezitaka Marekani na Iran kusitisha mapigano na kurejea kwenye meza ya mazungumzo. "Katibu Mkuu amekuwa na wasiwasi kwa muda sasa kwamba pande hizo mbili zisiporeje kwenye meza ya mazungumzo, wigo wa mzozo unaweza kupanuka, na inaonekana ndivyo hali ilivyo katika saa za hivi karibuni," Farhan Haq aliwaambia waandishi wa habari mjini New York. Kwa mujibu wake: "Kinachoendelea sio kitu kizuri - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa - anataka pande hizo kusitisha mapigano na kurejea tena kwenye juhudi za kidiplomasia." Msemaji huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aliongeza kusema: "Juhudi za upatanishi zinazofanywa na Pakistan, Qatar na nchi nyingine zinaendelea." Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye, azirai mahakamani Kizza Besigye, kiongozi wa upinzani nchini Uganda, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika mji mkuu Kampala baada ya kuanguka na kupoteza fahamu wakati wa kusikilizwa kwa kesi yake ya uhaini. Besigye, mwenye umri wa miaka 70, amekuwa kizuizini tangu mwezi Novemba 2024. Wakili wake mkuu alikamatwa mwezi uliopita na kushtakiwa kwa madai ya kushindwa kuripoti vitendo vya uhaini na anazuiliwa na polisi hadi sasa. Besigye ambaye hali yake ya afya inaonekana kuwa dhaifu, alikuwa akipinga uamuzi wa mawakili wa serikali kuteuliwa kumwakilisha mahakamani, kabla ya kuanguka na kupoteza fahamu. Walinzi wa gereza walimkimbiza hospitalini. “Bado amepoteza fahamu. Hawezi kuzungumza, na haitikii hata akidungwa sindano ili kupima mwitikio wa maumivu,” mkewe, Winnie Byanyima, ambaye anaongoza shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana ugonjwa wa UKIMWI (UNAIDS), amechapisha kwenye mtandao wa X. Siku ya Jumatano katika Mahakama Kuu ya Kampala, mashahidi waliokuwa mahakamani walisema Besigye alipaza sauti mara kadhaa akisema “wacheni” kuhusu suala la uwakilishi wake wa kisheria kabla ya kuanguka. Besigye alipelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Rufaa ya Mulago, hospitali kubwa zaidi ya umma nchini Uganda, lakini alikataa kutibiwa na wahudumu wa afya wa serikali. Mkewe Byanyima alisema kupitia X kuwa “Hatutaruhusu afisa yeyote wa serikali kumgusa.” Mkewe anataka Besigye aruhusiwe kupata matibabu kutoka kwa daktari wake binafsi katika kliniki ya kibinafsi, badala ya kutibiwa katika kituo cha afya cha serikali. Kitengo cha ICU ambako Besigye anatibiwa, kimezingirwa na maafisa wa usalama . Ripoti zinaeleza kuwa dada yake, ambaye pia ni daktari wake binafsi, ameweza kuruhusiwa kumwona. Wakili mkuu wa Besigye, Erias Lukwago, yuko gerezani baada ya kukamatwa na jeshi mwezi uliopita. Wakili wake mwingine Martha Karua kutoka nchini Kenya, alizuiwa kuingia nchini Uganda baada ya kusafiri kwenda huko mwezi uliopita kumwakilisha Besigye. Mwanawe Besigye, Adam Ampa, amemwomba Rais Yoweri Museveni na mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye ni mkuu wa jeshi la Uganda, kuwa na huruma na kumuachilia baba yake kwa misingi ya kibinadamu. Besigye, ambaye amewania urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni mara nne, alitekwa nyara nchini Kenya mwaka wa 2024. Jeshi la Iran (IRGC) limetangaza kuwa Mlango bahari wa Hormuz hauwezi kufunguliwa tena iwapo vitisho na kauli za vita bado zinatolewa na viongozi wa Marekani, pamoja na kuingilia harakati za meli katika eneo hilo. Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali la Iran, IRNA, jeshi hilo limesema,“Vitisho na uingiliaji vimeifanya hali kuwa ngumu na tata zaidi.” Taarifa hiyo pia ilisema, bila kuitaja nchi yoyote kwa jina, kwamba nchi zinazohusika kuisaidia Marekani katika mashambulizi yake yatakabiliwa vikali. Hapo jana CENTCOM ilitangaza kwamba IRGC hawana mamlaka ya kuamua njia ambayo meli zinapaswa kutumia katika Mlango bahari wa Hormuz. Watu 3 wauawa, 2 wajeruhiwa katika shambulio la Marekani katika kisiwa cha Qeshm, Iran Shirika la habari la Iran, Fars News Agency, limeripoti kuwa watu watatu wameuawa na wengine wawili kujeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani yaliyofanyika asubuhi ya leo katika Kisiwa cha Qeshm. Kulingana na maafisa wa afya, mama, baba na mtoto wao mwenye umri wa miaka miwili waliuawa katika shambulio lililolenga nyumba yao katika eneo la Chahtangu, mjini Qeshm. Kulingana na BBC Persian, watoto wengine wawili waliokuwa ndani ya nyumba hiyo walijeruhiwa na wamepelekwa hospitalini kupokea matibabu. Kenya power yatangaza kurejea kwa umeme baada ya huduma hiyo kukatika maeneo mengi nchini Kenya Shirika la kusambaza umeme nchini Kenya, Kenya Power, imetangaza kuwa umeme umerejea kikamilifu kwa wateja wake wote walioathiriwa na kukatika kwa huduma za umeme katika maeneo mbalimbali nchini Kenya usiku wa jana. Katika taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo mapema leo asubuhi, kampuni hiyo ilisema umeme umerejeshwa kikamilifu. “Tunafurahi kuwafahamisha kwamba usambazaji wa umeme ulirejeshwa kikamilifu kwa wateja wote walioathirika” Kupotea kwa kwa umeme kulishuhudia jijini Nairobi,maeneo ya pwani ya Kenya, Kati mwa Kenya na Bonde la Ufa. Kampuni hiyo katika taarifa yake ilidokeza kuwa kulikuwa na hitilafu za kimitambo, lakini imethibitisha kuwa huduma ya umeme sasa imerejea katika maeneo yote yaliyoathirika. Watu 8 wafariki ikiwemo watoto baada ya Urusi kuishambulia Ukraine Watu nane, wakiwemo watoto wawili, wamefariki katika mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyorushwa na Urusi nchini Ukraine. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, amesema kwamba Urusi inajiandaa kwa “shambulizi kubwa”, na kuwataka wananchi kuzingatia tahadhari na ving’ora vya mashambulizi ya anga. Mapema leo asubuhi, jeshi la Ukraine limeripoti mashambulizi kadhaa ya makombora na ndege zisizo na rubani katika maeneo mbalimbali nchini humo. Mashambulizi hayo yamefanyika baada ya Zelensky kukutana na Rais wa Marekani Donald Trump mjini Washington DC wiki hii, ambapo aliiomba Marekani kuipa Ukraine leseni ya kutengeneza mfumo wa makombora ya kuzuia mashambulizi ijulikanayo kama Patriot. Wasichana wawili wenye umri wa miaka 5 na 12 ni miongoni mwa watu sita waliofariki katika kijiji kilicho karibu na mji wa Kryvyi Rih, katikati mwa Ukraine, baada ya kombora la balistiki kulenga nyumba yao. Watu wengine wanane wamejeruhiwa, wakiwemo watoto wawili, huku maafisa wakionya kuwa idadi ya waliojeruhiwa na waliopoteza maisha inaweza kuongezeka. Mjini Kyiv, mtu mmoja alifariki na moto kuzuka katika majengo matatu yasiyo ya makazi usiku kucha, Meya wa mji huo Vitali Klitschko alichapisha kwenye Telegram. Jeshi la Marekani lasema limelenga kambi za kijeshi za Iran katika wimbi jipya la mashambulizi Kituo kikuu cha kundesha oparesheni za kijeshi nchini Marekani CENTCOM, kimetangaza kumaliza mashambulizi yake dhidi ya Iran yaliyofanyika mapema leo asubuhi, ambayo yalikuwa yakijibu mashambulizi ya makombora ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani nchini Jordan. Mashambulizi hayo yalimalizika karibu mwendo wa saa kumi na moja asubuhi kwa saa za Iran. Kulingana na taarifa ya CENTCOM, mashambulizi hayo yalilenga maeneo walioko wanajeshi wa Iran (IRGC), yakiwemo vituo vya uongozi wa kijeshi, maeneo ya kuhifadhi makombora na ndege zisizo na rubani, vituo vya ufuatiliaji na ulinzi wa pwani, pamoja na uwezo wa kijeshi wa majini nchini Iran. CENTCOM imesema lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kupunguza zaidi vitisho kutoka Iran na washirika wake dhidi ya wanajeshi wa Marekani na meli za kibiashara za mataifa jirani. Hata hivyo, mamlaka za eneo la Qeshm zimesema leo asubuhi nyumba moja yenye angalau wakazi watatu katika kisiwa hicho ililengwa katika mashambulizi hayo. Mamlaka hizo pia zilitoa picha zinazoonyesha waokoaji wakijaribu kuwafikia watu waliokuwa wamenaswa chini ya vifusi. Idadi ya waliofariki kwa tetemeko la ardhi yafikia 30 nchini Japan Idadi ya watu waliofariki baada ya tetemeko kubwa la ardhi lililotokea kusini magharibi mwa Japan imeongezeka hadi 30, kulingana na mamlaka za taifa hilo. Waokoaji bado wanaendelea na shughuli za kutafuta manusura baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 6.8 katika kipimo cha Richter kushuhudiwa katika mkoa wa Kumamoto, katika kisiwa cha Kyushu, siku ya Jumanne na kusababisha uharibifu mkubwa wa nyumba na miundombinu. Maelfu ya wakazi waliolazimika kuondoka kwenye makazi yao sasa wanaishi katika vituo vya muda vya kuwahifadhi waathirika. Kulingana na utabiri wa hali ya hewa, joto katika mkoa huo unaweza kufikia nyuzi joto 39 katika siku zijazo, huku maafisa wamewataka manusura na waokoaji kuchukua tahadhari dhidi ya kiharusi cha joto. Zaidi ya mitetemeko 100 ya kufuatia tetemeko kuu imerekodiwa tangu tetemeko la kwanza lilipotokea. Baadhi ya wakazi wameamua kulala kwenye magari yao kwa hofu ya kutokea kwa mitetemeko mingine. WAFCON 2026: Kenya na Tanzania kusaka heshima Morocco Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) inaendelea leo huku macho yakielekezwa kwa timu za Afrika Mashariki, ambapo Kenya itashuka dimbani leo Alhamisi dhidi ya Senegal, wakati Tanzania itacheza kesho Ijumaa dhidi ya Burkina Faso. Kenya itavaana na Senegal kwenye Uwanja wa Olympic mjini Rabat, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika Kundi A baada ya kupoteza mechi ya ufunguzi 4-0 dhidi ya wenyeji Morocco. Kwa upande wa Tanzania, Twiga Stars itacheza na Burkina Faso kuanzia katika Uwanja wa Larbi Zaouli mjini Casablanca, ikiwa na lengo la kuendeleza mwanzo mzuri baada ya kushinda mchezo wake wa kwanza 2-1 dhidi ya Afrika Kusini. Mbali na mchezo wa Kenya, leo pia kutakuwa na pambano kali la Kundi A kati ya wenyeji Morocco na Algeria, litakaloanza mjini Rabat. Katika michezo iliyochezwa Jumatano, Ghana ilianza kampeni yake kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde katika Kundi D. Nayo Cameroon iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mali katika mchezo mwingine wa Kundi D. Matokeo ya mechi za ufunguzi kwa Kenya na Tanzania Ushindi wa Tanzania dhidi ya Afrika Kusini umeiweka Twiga Stars katika nafasi nzuri ya kusaka tiketi ya hatua ya robo fainali, huku Kenya ikihitaji matokeo mazuri dhidi ya Senegal ili kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo. Liverpool yaandaa ofa ya kwanza kumsajili Barcola kutoka PSG Liverpool imeongeza juhudi zake za kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, na inajiandaa kuwasilisha ofa yake ya kwanza kwa klabu hiyo ya Ufaransa. Barcola, mwenye umri wa miaka 23, ametajwa kuwa chaguo kuu la Liverpool katika harakati za kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah, aliyeondoka mwishoni mwa msimu uliopita. PSG inasema thamani ya mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa ni pauni milioni 145. Iwapo usajili huo utakamilika kwa kiasi hicho, utavunja rekodi ya uhamisho ghali zaidi kuwahi kufanyika nchini Uingereza. Hata hivyo, viongozi wa Liverpool wana matumaini ya kufikia makubaliano kwa ada inayokaribia pauni milioni 100. Barcola amebakiza miaka miwili katika mkataba wake na PSG, lakini inaelezwa kuwa yuko tayari kuhamia Liverpool akitafuta changamoto mpya, baada ya nafasi yake katika kikosi cha kwanza cha mabingwa hao wa Ufaransa kupungua. Awali, Liverpool ilikuwa ikimwania winga wa RB Leipzig Yan Diomande, lakini sasa mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na Real Madrid. Barcola alikuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kilichofika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia la 2026. Marekani yashambulia tena Iran, Trump aahidi mashambulizi makali zaidi Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya dhidi ya Iran usiku wa Alhamisi, likisema ni hatua ya kujibu shambulio lililolenga wanajeshi wake walioko Mashariki ya Kati mapema wiki hii. Haya ni mashambulizi ya kwanza ya Marekani dhidi ya Iran katika takriban wiki moja. Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti milipuko karibu na Kisiwa cha Qeshm na mji wa Abadan, kusini mwa nchi hiyo. Shirika la habari la serikali ya Iran, IRNA, limemnukuu afisa wa jimbo la Hormozgan akisema kuwa vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta watu wawili wanaodaiwa kufunikwa na vifusi baada ya kuangukiwa na nyumba katika Kisiwa cha Qeshm. Mashambulizi hayo yamefanyika saa chache baada ya Rais wa Marekani Donald Trump kuahidi kuijibu Iran kwa "nguvu kubwa", kufuatia shambulio ambalo Tehran inadaiwa kulenga wanajeshi wa Marekani walioko Mashariki ya Kati. Siku ya Jumatano, jeshi la Marekani na lile la Jordan yalisema yalizuia makombora yaliyokuwa yamerushwa kuelekea Jordan, yakidai yalitoka Iran na yalilenga maeneo yenye wanajeshi wa Marekani. Katika taarifa yake, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema mashambulizi hayo ni "jibu kali" kwa kile ilichokiita mashambulizi ya Iran dhidi ya wanajeshi wa Marekani yaliyodhibitiwa siku iliyotangulia. Wakati huo huo, tovuti ya habari ya Marekani Axios, ikimnukuu afisa wa Marekani ambaye haikumtaja kwa jina, ilisema Washington ilikuwa imeanzisha mashambulizi ya anga dhidi ya Iran. Awali akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ya White House, Trump alisema Marekani itaishambulia Iran "kwa nguvu kubwa". "Sasa ni zamu yetu," alisema Trump, huku akiongeza kuwa bado kuna uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano siku zijazo, lakini akasisitiza kuwa, "tutaishambulia kwa nguvu sana."

How it works

Once you click Generate, Ollama reads this article and crafts 5 comprehension questions. Your answers are graded against the article content — general knowledge won't be enough. Score 70+ to count toward your certificate.

Questions are cached — you'll always get the same 5 for this article.