general4428 wordsRead on Arc Codex

Shambulio la Iran lavuruga shughuli za meli za kivita za Marekani

Moja kwa moja, Shambulio la Iran lavuruga shughuli za meli za kivita za Marekani Ripoti hiyo imeongeza kuwa hali hiyo imesababisha upungufu wa baadhi ya mahitaji na kuongeza mzigo kwa wanajeshi wanaohudumu kwenye meli zinazofanya operesheni katika eneo hilo. Muhtasari - Rais Ramaphosa akemea unyanyasaji wa wageni Afrika Kusini, asema ni aibu - Shambulio la Iran lavuruga usambazaji wa mahitaji kwa meli za kivita za Marekani - Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi afanya mabadiliko ya Makamanda wakuu jeshini - Iran yaishutumu Qatar kuwashikilia marubani watatu wa Iran - Nchi na mashirika ya kimataifa zaitaka DRC na Rwanda kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya amani - Ebola inasambaa kwa kiwango cha 'kutisha sana' DR Congo, WHO yaonya - TAZAMA: Majengo yaporomoka Indonesia baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 7.7 - BBC yaomba mahakama kuwashurutisha wanafamilia wa Trump kutoa ushahidi katika kesi ya Panorama - Kiongozi wa upinzani Zambia Mundubile ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais kabla matokeo rasmi - Jason Arday, Profesa wa zamani wa Cambridge aliyekabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, apatikana amefariki dunia - Burundi yapokonywa haki ya kuandaa mashindano ya magari ya kimataifa mwaka huu - Arsenal wanalenga kuanza msimu kwa ushindi mkubwa - Meli ya kivita ya Marekani yaelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya USS Abraham Lincoln - Watu wanne wauawa katika shambulizi la makombora la Wahouthi nchini Yemen - 'Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa na utaendelea kuwa wa Iran' - Kazem - Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani Moja kwa moja Na Mariam Mjahid & Leila Mohammed Nguruwe zaidi ya 1000 wafariki Kenya kutokana na mlipuko wa Homa ya Nguruwe Wakulima nchini Kenya wanaendelea kukadiria hasara baada ya mlipuko wa Homa ya Nguruwe kusababisha vifo vya takriban nguruwe zaid ya 1000. Kulinganana idara ya Idara ya huduma kwa Mifugo nchini Kenya, Jimbo la Kiambu limeathirika pakubwa na mlipuko huo ambao umeathiria wafugaji zaidi ya ishirini katika miji ya Juja, Thika na Ruiru. Idara hiyo ya huduma kwa mifugo imesema kwamba mlipuko wa aina ya Homa ya Nguruwe inayopatikana barani Africa ilitambuliwa kwanza Mwezi Mei mwaka huu, huku nguruwe takriban 1,470 wakiripotiwa kuwa wagonjwa au kufariki huku baadhi ya wafugaji wakisema kwamba mifugo wao walifariki katika muda mfupi wa kuthibtihiswa kuuguwa Homa ya Nguruwe. Mlipuko unaoshuhudiwa katika Jimbo la Kiambu haujaripotiwa kwengineko nchini Kenya kwa sasa, ila umeweka wazi udhaifu uliopo katika mfumo w auchunguzi wa maradhi nchini Kenya. Serikali ya Kenya imeweka mikakati ya kudhibiti kusambaa kwa mlipuko wa sasa huku ikijiweka juhudui zote kukabiliana na kuenea kwa ugonjw ahuo kwa wakulima/wafugaji ambao wako katika maeneo yaliyoathirika.Hata hivyo, mamlaka nchini humo zimeonya kwamba wakulima huenda wakapata hasara kubwa ikiwa hali haitathibitiwa kwa haraka. Mkurugenzi wa idara ya huduma za afya kwa mifugo, katika wizara ya Kilimo na Ufugaji nchini Kenya, Dkt. Allan azegele amesema kwamba aina hii ya Homa ya Nguruwe {ASF} inaambukizwa kwa haraka sana na inasambaa pia kwa kasi miongoni mwa nguruwe huku viwango vya mifugo wanaofariki kutokana na ugonjw ahuo ikiwa asilimia 70 kulingana na umri wa mnyama na uwezo wake kupambana na maradhi mwilini mwake. Soma Pia: Watu 11 wauawa katika Shambulio la Israel kusini mwa Lebanon Watu 11 wameuawa katika mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon, kulingana na maafisa, katika mojawapo ya siku zenye vifo vingi zaidi tangu makubaliano ya kupunguza uhasama yalipotangazwa mwezi Juni. Waziri Mkuu wa Lebanon alisema watu saba waliuawa katika shambulio dhidi ya nyumba moja nje kidogo ya mji wa Ansar katika wilaya ya Nabatieh; vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa miongoni mwa waliouawa kulikuwa na watoto watatu na wanawake wawili. Baadaye Jumamosi, mfululizo mwingine wa mashambulizi ulilenga mji wa Deir al-Zahrani, na kuua watu wanne huku wengine watano wakijeruhiwa, Wizara ya Afya ya Lebanon ilisema. Jeshi la Israel lilisema lilishambulia "miundombinu ya kigaidi ya Hezbollah" ikiwa ni jibu kwa hatua iliyochukuliwa awali dhidi ya askari wake. Maafisa wanasema shambulio hilo huko Ansar, lililotokea majira ya saa 04:30 (01:30 GMT), lililenga eneo ambalo familia zilizokimbia makazi yao zilikuwa zikiishi. Picha kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha mawingu makubwa ya moshi yakitanda mitaani huku ving'ora vikilia. Waziri Mkuu wa Lebanon, Nawaf Salam, alilaani mashambulizi hayo, akisema raia hao saba waliouawa hawakuwa "miundombinu ya kijeshi". "Ni lazima Israel ikomeshe ongezeko hili la uhasama," alisema. "Kwa maana usalama wa watu wetu na haki yao ya kuishi katika ardhi yao haviko tayari kwa majadiliano au biashara ya kisiasa." Jeshi la Israel (IDF) lilisema tukio lililosababisha shambulio lake huko Ansar lilitokea katika eneo la Ali al-Taher Ridge, eneo la kimkakati lenye mwinuko linalotazamana na sehemu kubwa ya kusini-mashariki mwa Lebanon na ambalo ni mojawapo ya maeneo yanayopiganwa vikali zaidi katika vita hivyo. Shirika la Habari la Taifa la Lebanon (NNA) pia liliripoti mfululizo wa mashambulizi karibu na eneo hilo la mwinuko. Karibu na mpaka, nyumba kadhaa ziliripotiwa kuharibiwa huko Bint Jbeil, huku vikosi vya Israel vikifyatua risasi nzito za bunduki kuelekea kwenye nyumba, kulingana na NNA. Lebanon ilijikuta ikivutwa katika vita kati ya Israel, Marekani na Iran mnamo tarehe 2 Machi, wakati Hezbollah - kundi lenye silaha linaloungwa mkono na Iran - liliporusha roketi kuelekea Israel ikiwa ni kulipiza kisasi kwa shambulio lililomuua kiongozi mkuu wa Iran. Israel ilijibu kwa kuanzisha kampeni ya mashambulizi ya anga kote Lebanon na kuvamia sehemu kubwa ya kusini mwa nchi hiyo. Vikosi vyake vinaendelea kukalia takriban asilimia 5 ya eneo la Lebanon. Rais Ramaphosa akemea unyanyasaji wa wageni Afrika Kusini, asema ni aibu Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa amesema nchi hiyo ina wasiwasi na inaona aibu kutokana na namna raia wa kigeni, wakiwemo wahamiaji kutoka mataifa mengine ya Afrika, wanavyonyanyaswa nchini humo. Akizungumza kabla ya mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC, Ramaphosa amelaani ubaguzi, vitisho na vurugu dhidi ya wahamiaji, akisema Afrika Kusini haiwezi kuzungumzia umoja wa Afrika wakati raia wa mataifa mengine ya Afrika wanadhalilishwa. "Katika nchi yetu, tunapaswa kuhuzunika sana na kuona aibu kwamba watu kutoka mataifa mengine, ambao baadhi ya viongozi wao wako hapa, wametendewa vibaya na hata kulazimishwa kuondoka nchini kutokana na vitisho vya vurugu," alisema Ramaphosa. Amesema vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na watu wachache vinakinzana na misingi ya mshikamano ambayo jumuiya ya SADC imejengwa juu yake. Kauli ya Ramaphosa inakuja wakati kukiwa na mvutano mpya kuhusu uhamiaji na chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini, huku zaidi ya wahamiaji 178,000 kutoka mataifa ya Afrika wakiripotiwa kuondoka au kurejeshwa katika nchi zao katika miezi ya hivi karibuni. Pia unaweza kusoma: Shambulio la Iran lavuruga usambazaji wa mahitaji kwa meli za kivita za Marekani Mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani ya Iran dhidi ya kituo cha wanamaji wa Marekani nchini Bahrain yamevuruga mfumo wa usambazaji wa mahitaji kwa meli ya kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, pamoja na meli nyingine za Marekani katika eneo hilo, kwa mujibu wa gazeti la New York Times. Gazeti hilo limesema shambulio hilo liliharibu kituo muhimu cha kuhifadhi na kusambaza mahitaji kinachotumiwa na Jeshi la Wanamaji la Marekani, hali iliyolazimisha Pentagon kuongeza utegemezi wake kwa kituo cha kijeshi cha mbali cha Diego Garcia katika kuendesha operesheni zake za majini. Ripoti hiyo imeongeza kuwa hali hiyo imesababisha upungufu wa baadhi ya mahitaji na kuongeza mzigo kwa wanajeshi wanaohudumu kwenye meli zinazofanya operesheni katika eneo hilo. USS Abraham Lincoln imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kwa takriban miezi tisa, huku USS George Washington ikitarajiwa kuchukua nafasi yake hivi karibuni. Soma zaidi: Mkuu wa jeshi la Uganda Jenerali Muhoozi afanya mabadiliko ya Makamanda wakuu jeshini Mkuu wa Jeshi la Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametangaza mabadiliko katika uongozi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda, UPDF. Katika mabadiliko yaliyotangazwa Jumamosi, Jenerali Kainerugaba amewahamisha makamanda wakuu wa Jeshi la Nchi Kavu, kikosi cha askari wanaopigana kwenye nchi kavu na Kikosi cha Akiba. Tangazo hilo limetolewa wiki moja kabla ya aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Akiba, Luteni Jenerali Charles Otema Awany, kustaafu. Meja Jenerali Joseph Ssemwanga, aliyekuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu, ameteuliwa kuwa Afisa Mkuu na Kamanda wa Kikosi cha Akiba, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Luteni Jenerali Otema. Meja Jenerali Felix Busizoori, aliyekuwa Kamanda wa Divisheni ya Nne ya kikosi cha nchi kavu, sasa ameteuliwa kuwa Naibu Kamanda wa Jeshi la Nchi Kavu, akichukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na Meja Jenerali Ssemwanga. Kwa upande wake, Meja Jenerali Wilberforce Sserunkuma, aliyekuwa Kamanda wa Divisheni ya Tatu ya kikosi cha nchi kavu, ameteuliwa kuwa Kamanda wa Divisheni ya Nne ya kikosi hicho. Mabadiliko hayo yanaanza kutekelezwa mara moja, kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma wa UPDF, Kanali Chris Magezi. Mabadiliko hayo yanakuja wakati UPDF ikijiandaa kwa kustaafu kwa Luteni Jenerali Otema wiki ijayo. Iran yaishutumu Qatar kuwashikilia marubani watatu wa Iran Mkuu wa Kamati ya Kutafuta Watu Waliopotea ya Kamandi Kuu ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa marubani watatu wa Iran wanashikiliwa na Qatar, na kuitaka Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu, ICRC, kusaidia kufafanua hali yao. Brigedia Jenerali Mohammad Bagherzadeh amemtumia barua Marianna Spoliarik, mkuu wa ICRC, akisema kuwa ndege mbili za kivita aina ya Su 24 ziliondoka tarehe 2 Machi 2026 kwa ajili ya kutekeleza operesheni ya kijeshi dhidi ya kituo cha kijeshi cha adui nchini Qatar. Amesema wakati ndege hizo zikirejea, marubani waliruka kutoka kwenye ndege hizo baada ya kushambuliwa na mifumo ya ulinzi wa anga ya adui. Mmoja kati ya marubani hao wanne, Majid Kazemi, alizikwa mjini Shiraz Ijumaa, Agosti 29. Hata hivyo, kwa mujibu wa Brigedia Jenerali Bagherzadeh, marubani wengine watatu walikamatwa wakiwa hai na vikosi vya Qatar. Ametaja majina yao kuwa Javad Salehi, Abdul Majid Dashtian na Imran Behroshian. Awali, mamlaka na vyombo vya habari nchini Iran vilikuwa vikiripoti kuhusu juhudi za kubaini hatima ya marubani hao watatu. Soma Zaidi: Nchi na mashirika ya kimataifa zaitaka DRC na Rwanda kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya amani Wadau wanaohusika katika mchakato wa amani wa Ukanda wa Maziwa Makuu wanazitaka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Rwanda kutekeleza kwa haraka ahadi zao chini ya makubaliano ya amani, huku juhudi zikiendelea kwa lengo la kurejesha utulivu na kutatua suala la makundi yenye silaha mashariki mwa DRC. Wito huo ulitolewa wakati wa mkutano wa sita wa Mfumo wa Pamoja wa Usalama na Uratibu (JSCM), ambao hufuatilia utekelezaji wa makubaliano ya amani kati ya DRC na Rwanda. Mkutano huo uliwakutanisha wawakilishi wa nchi hizo, pamoja na wawakilishi kutoka Marekani, Qatar, Togo -kama mpatanishi wa Kiafrika-, na Umoja wa Afrika {AU}. Katika mkutano huo uliofanyika Geneva nchini Uswizi, tarehe 12 na 13 Agosti, DRC na Rwanda zilikubaliana kuendeleza miradi miwili inayolenga kuendelea kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa Makubaliano ya Washington. Washiriki kwenye mchakato huo wa amani pia walijadili mpango wa DRC wa kuwapokonya silaha na kuwarejesha katika maisha ya kawaida wapiganaji wa kundi la FDLR. Kundi linalofuatilia mchakato huo kutoka Ulaya na Marekani (ICG) limepokea vyema jinsi utekelezaji wa Makubaliano ya Washington unavyoendelea. Katika taarifa yake, kundi hilo ambalo linajumuisha Marekani, Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Ufaransa, Ujerumani, Uholanzi, Uswizi, Uswidi na Uingereza lilikaribisha makubaliano yaliyotiwa saini tarehe 28 Julai na kundi la waasi la FDLR (Vikosi vya Kidemokrasia vya Ukombozi wa Rwanda), ambalo lilikubali kuweka chini silaha, kuvunja vikosi vyake na kuwarejesha wapiganaji wake katika jamii. ICG inazitaka mamlaka za DRC kuandaa mpango madhubuti na ratiba iliyo wazi kwa ajili ya kuliondoa kabisa kundi la FDLR, kwa mujibu wa makubaliano ya amani yaliyopo. Kundi hilo linasisitiza kuwa serikali ya Kinshasa inapaswa kueleza wazi jinsi wale waliofanya uhalifu watakavyowajibishwa, na kushirikiana kwa karibu na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO). Aidha, Linakumbusha kuwa kushirikiana kwa namna yoyote ile na wapiganaji wa FDLR hakulingani na ahadi za DRC chini ya Makubaliano ya Washington. Hayo yakijiri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imefungua kesi dhidi ya Rwanda katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki mjini The Hague, ikiitaka mahakama hiyo kuiwajibisha Rwanda kwa madai ya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa. Hadi sasa, mamlaka za Rwanda hazijatoa tamko kuhusu kesi hiyo. Hata hivyo, wachambuzi wa sheria za kimataifa wanasema kesi hiyo inaweza kukabiliwa na changamoto za kisheria kuhusu mamlaka ya mahakama kuisikiliza bila ridhaa ya Rwanda au msingi mwingine wa kisheria unaoifunga nchi hiyo. Soma Zaidi: Ebola inasambaa kwa kiwango cha 'kutisha sana' DR Congo, WHO yaonya Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa tahadhari kuhusu hatari ya kuenea kwa Ebola kuvuka mipaka baada ya ugonjwa huo kugunduliwa katika jimbo la sita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Maafisa wanasema Uganda bado iko hatarini, hata wakati huu inapopitia kipindi cha ufuatiliaji cha siku 42 baada ya mgonjwa wa mwisho aliyepata maambukizi kutoka nje kuruhusiwa kutoka hospitalini. WHO imesema kwamba mlipuko wa Ebola uliothibitishwa kuwepo Mashariki mwa Congo mwezi Mei mwaka huu wa 2026 unaenea kwa kasi, huku maambukizi yakifikia hatua yake ya juu zaidi. Awali, maafisa wa WHO walionya kuwa mlipuko huo unaosababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo unaelekea kuwa janga kubwa zaidi la Ebola kuwahi kurekodiwa. Kufikia sasa, zaidi ya visa 4,700 na vifo zaidi ya 2,000 vimeripotiwa. Wanasema ongezeko la haraka la visa hivyo linaongeza hatari ya ugonjwa huo kusambaa katika nchi jirani kupitia harakati za kuvuka mipaka zinazochochewa na ukosefu wa usalama na mgogoro wa kibinadamu unaoendelea mashariki mwa DRC. Hali hii imeifanya Uganda kuimarisha ufuatiliaji katika mpaka wake wa magharibi. Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi. Virusi vya Ebola kwa kawaida huwapata wanyama, hasa popo, lakini binadamu huambukizwa wakati pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa. Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu. Maelezo zaidi: TAZAMA: Majengo yaporomoka Indonesia baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 7.7 Takriban watu 20 wamefariki dunia nchini Indonesia baada ya tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 7.7 kukumba kisiwa cha Flores mapema Jumamosi. Shirika la Kitaifa la Kukabiliana na Majanga la Indonesia, BNPB, limesema idadi hiyo ni ya awali huku shughuli za uokoaji na utafutaji wa manusura zikiendelea. Tetemeko hilo lilisababisha kuporomoka kwa majengo na miundombinu kadhaa, huku mitetemeko mingine ikifuatia, ikiwemo mmoja wenye ukubwa wa 6.1. Video kutoka bandarini Maumere ilionyesha vipande vikubwa vya vifusi vikianguka kutoka kwenye jengo la kituo cha abiria na kuwapiga watu waliokuwa wakisubiri kupanda kivuko. Baadhi ya watu walitupwa baharini baada ya daraja la kuingilia kwenye kivuko kuporomoka. Arnold Welianto, mkazi wa Talibura, kijiji kilicho karibu na pwani huko Sikka, East Nusa Tenggara, alisema alishtuliwa usingizini na "tetemo kali sana", akiongeza: "Nilishtuka na kuamka, kisha nikakimbilia chumbani kwa mtoto wangu mara moja." Gavana wa East Nusa Tenggara, Emanuel Melkiades Laka Lena, amesema baadhi ya waathiriwa walifariki baada ya kuangukiwa na vifusi vya majengo yaliyoporomoka. Tetemeko hilo lilitokea katika kina cha takriban kilomita 15, kulingana na shirika la hali ya hewa na jiolojia la Indonesia. Onyo la tsunami lilitolewa baada ya tetemeko hilo, na kusababisha wakazi kukimbilia maeneo ya juu na ya ndani. Hata hivyo, onyo hilo liliondolewa takriban saa tatu baadaye baada ya kutogundulika ongezeko kubwa la kina cha maji baharini. Mamlaka zimesema takriban watu 2,000 walihama au kuondoka katika maeneo yao kwa hiari kufuatia tetemeko hilo. Mbali na vifo, watu kadhaa wamejeruhiwa, huku wawili wakiwa katika hali mbaya na wengine 11 wakipata majeraha madogo. Soma Zaidi: BBC yaomba mahakama kuwashurutisha wanafamilia wa Trump kutoa ushahidi katika kesi ya Panorama BBC imeiomba mahakama idhini ya kupata - amri rasmi ya mahakama yaani subpoena - inayowataka wanafamilia wa Donald Trump kutoa nyaraka na ushahidi, huku ikijitetea dhidi ya kesi ya madai ya kashfa ya dola bilioni 10 (pauni bilioni 7.4) iliyofunguliwa na rais huyo wa Marekani dhidi ya shirika hilo la utangazaji. Nyaraka za mahakama zinaonyesha kuwa wawakilishi wa timu ya kisheria inayoiwakilisha BBC katika kesi hiyo walijaribu mwezi Mei kuwasilisha amri hizo kwa mwana wa rais, Donald Trump Jr, binti yake Ivanka Trump, na mkwe wake Jared Kushner. Rais huyo ameifungulia BBC kesi hiyo kutokana na kipindi cha *Panorama* ambacho kilichanganya sehemu mbili tofauti za hotuba aliyoitoa kabla ya ghasia za Capitol mwaka 2021. Katika hati ya hivi karibuni iliyowasilishwa mahakamani, mawakili wa BBC wanahoji kuwa wanafamilia wa Trump walikuwa na "ufahamu wa kibinafsi" kuhusu nia yake ya kutoa hotuba hiyo, jambo linalofanya ushahidi na nyaraka zao kuwa muhimu katika kesi ya madai ya kashfa iliyofunguliwa na rais huyo. Ikirejelea ushahidi uliokusanywa awali na kamati ya Bunge la Marekani, hati hiyo inaeleza kuwa Donald Trump Jr na Ivanka Trump walikuwepo wakati baba yao akirekebisha na kutoa hotuba hiyo, na kuongeza kuwa Jared Kushner alimwandalia rasimu ya taarifa ambayo ingelaani matumizi ya vurugu. Hati hiyo inaomba mahakama kuruhusu hati za amri ya wito wa kutoa ushahidi (subpoenas) zitumwe kwa barua pepe na barua iliyosajiliwa (certified mail), ikibainisha kuwa majaribio ya kuzifikisha hati hizo kwa mkono hayakufanikiwa. Katika tukio moja, kulingana na hati hiyo, mwakilishi wa timu ya mawakili wa BBC alijaribu kufikisha hati ya wito kwa ajili ya Ivanka Trump na Jared Kushner nyumbani kwao Florida, lakini alizuiwa kuingia katika kituo cha ukaguzi cha polisi na baadaye akaambiwa na kitengo malaum cha ulinzi wa rais cha Marekani (Secret Service) kuwa hawaezi kupokea hati hizo. Vilevile, kulingana na hati hiyo, mwakilishi alijaribu kufikisha hati ya wito kwa Donald Trump Jr katika jengo la Trump Tower jijini New York lakini akaambiwa na mfanyakazi wa mapokezi kuwa mtu ambaye kwa kawaida hupokea nyaraka kama hizo huenda alikuwa mapumzikoni kwa ajili ya chakula cha mchana. Katika jaribio jingine siku mbili baadaye, mwakilishi huyo aliambiwa kuwa "idara ya sheria" haikuwepo siku hiyo, kulingana na hati hiyo. BBC tayari iliomba radhi kwa kuhariri hotuba hiyo, lakini imekanusha kwamba uhariri huo unahalalisha madai ya kashfa yaliyowasilishwa na Trump. Mawakili wa Trump wameombwa kutoa maoni kuhusu hatua hiyo ya BBC. Soma Zaidi: Kiongozi wa upinzani Zambia Mundubile ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa urais kabla matokeo rasmi Mgombea urais wa chama cha NRPUP nchini Zambia, Brian Mundubile, amewaonya Watanzania anaodai wamehusika katika siasa za Zambia, akiwataka kuondoka nchini humo. Mundubile amesema Zambia si Tanzania na kwamba mbinu za kisiasa zinazoweza kufanya kazi Tanzania haziwezi kutumika nchini Zambia. "Ndugu zangu Watanzania ambao mmekodiwa, tafadhali tokeni katika nchi yetu." Amesema chama tawala cha UPND hakiwezi kushinda uchaguzi huo na kukituhumu kutumia kile alichokiita "mbinu ya Tanzania" ili kupata ushindi. "UPND hawawezi kushinda uchaguzi huu, hakuna muujiza. Sasa wameamua kutumia mbinu ya Tanzania. Zambia si Tanzania. Hii ni Zambia. Wale wanaofikiri wanaweza kuingiza katika nchi hii mbinu inayofanya kazi Tanzania, hawawezi kufanikiwa kamwe." Kauli ya Mundubile imekuja wakati mchakato wa kuhesabu kura katika uchaguzi wa Zambia ukiendelea chini ya ulinzi mkali, baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kusimamisha kwa muda zoezi hilo kufuatia taarifa za mashambulizi dhidi ya maafisa wa uchaguzi na kuibwa kwa kura. Tume hiyo imesisitiza kuwa wagombea hawapaswi kujitangaza washindi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa. Mundubile, ambaye ni mmoja wa wagombea wakuu wa upinzani, tayari amejitangaza mshindi wa uchaguzi huo, licha ya Tume ya Uchaguzi ya Zambia kutokuwa imetangaza matokeo ya mwisho. Soma Zaidi: Jason Arday, Profesa wa zamani wa Cambridge aliyekabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, apatikana amefariki dunia Jason Arday, profesa wa zamani wa Chuo Kikuu cha Cambridge aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, amefariki dunia. Huduma za dharura zimesema mwanaume mmoja alipatikana akiwa hajitambui katika eneo la Battersea, kusini mwa London, Ijumaa alasiri. Arday alijiuzulu wiki iliyopita kutoka nafasi yake ya profesa wa sosholojia ya elimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, kufuatia tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma pamoja na maswali kuhusu baadhi ya mafanikio yake. Arday alikuwa amekanusha tuhuma hizo. Familia yake imesema katika taarifa kwamba ilikuwa "katika mshtuko" baada ya kumpoteza baba, mwenza, kaka, mjomba na mwana wao waliyemuelezea kuwa wa kipekee. Familia hiyo iliongeza: "Kampeni ya taarifa za kupotosha ilikuwa imemlemea Jason, ambaye alikuwa mtu mpole na ambaye daima alitaka kuona mazuri kwa kila mtu." Mapema Ijumaa, maafisa wa polisi waliitwa katika anwani hiyo iliyoko Battersea na Huduma ya Ambulance ya London. Katika taarifa, Polisi wa Metropolitan walisema: "Kwa wakati huu, kifo chake kinachukuliwa kuwa kisichotarajiwa, lakini haiaminiki kuwa kilitokana na mazingira ya kutatanisha." Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Profesa Deborah Prentice, amesema: "Tumehuzunishwa sana kusikia habari hizi za kusikitisha." Soma Zaidi: Burundi yapokonywa haki ya kuandaa mashindano ya magari ya kimataifa mwaka huu Shirikisho la Kimataifa la Michezo ya Magari, FIA, limeiondolea Burundi haki ya kuandaa mashindano ya magari ya Kimataifa iliyokuwa imepangwa kufanyika mjini Ngozi mwezi Agosti mwaka huu. Baadhi ya taarifa zilizopatikana na BBC Gahuza zinaeleza kuwa uamuzi huo umetokana na mapungufu ya kiutawala yaliyojitokeza katika taasisi ya Burundi iliyokuwa na jukumu la kuandaa mashindano hayo, pamoja na kasoro katika matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mashindano hayo. BBC Gahuzamiryango iliwasiliana na viongozi wa taasisi inayosimamia maandalizi ya Rally nchini Burundi ili kupata maelezo yao kuhusu suala hilo. Hata hivyo, hadi habari hii ilipochapishwa, hawakuwa wamejibu. Watu walio karibu na waandaaji pamoja na mashindano ya magari nchini Burundi wameithibitishia BBC kwamba FIA imeiondoa Burundi kwenye kalenda ya mashindano ya mwaka huu. Hata hivyo, vyanzo hivyo vimesema uamuzi huo umetokana na Burundi kutotekeleza wajibu wake wa kutoa mchango wa fedha unaohitajika kwa ajili ya kuandaa mashindano hayo. Mmoja wao alisema kila nchi inayoshiriki katika maandalizi ya mashindano hayo inapaswa kutoa kiasi fulani cha fedha kila mwaka. Amesema: "Iwapo nchi haijatoa fedha hizo, FIA huiondoa kwenye kalenda ya mashindano ili iweze kuelekeza fedha zake katika mashindano mengine." Kufutwa kwa mashindano hayo hakutaathiri washindani pekee, bali pia kunaweza kuwa pigo kwa wafanyabiashara mbalimbali, wakiwemo wamiliki wa nyumba za kulaza wageni. Wafanyabiashara hao wamekuwa wakinufaika na mashindano ya magari kwa kupokea idadi kubwa ya wageni kutoka maeneo mbalimbali ya Burundi pamoja na nchi nyingine. Kwa mfano, katika mashindano ya Kimataifa ya magari ya mwaka 2025, washiriki walitoka Burundi, Rwanda, Kenya, Tanzania, Uganda na Zambia. Arsenal wanalenga kuanza msimu kwa ushindi mkubwa Arsenal wataanza msimu mpya wakiwa na azma ya kuonyesha mapema kuwa wana uwezo wa kushindania mataji, baada ya msimu uliopita wenye matokeo mchanganyiko na changamoto kadhaa, huku shughuli zao kwenye soko la uhamisho zikianza kwa utulivu. Kikosi cha Mikel Arteta kilianza maandalizi ya msimu kwa ushindi mzuri dhidi ya MK Dons na Girona, kabla ya kupata vipigo kutoka kwa Real Betis na Borussia Dortmund. Arsenal walihitimisha maandalizi yao kwa sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Como ya Serie A nchini Italia. Nje ya uwanja, Arsenal wamekuwa na utulivu katika kipindi hiki cha kiangazi, huku usajili wa Bruno Guimaraes ukiwapa nguvu zaidi baada ya kuimarisha safu yao ya kiungo. Iwapo Arsenal wataifunga Manchester City, ambayo inaanza enzi mpya baada ya kuondoka kwa Pep Guardiola, ushindi huo utakuwa ujumbe kwamba bado ni moja ya timu zinazopaswa kuogopwa na wapinzani wao katika mbio za ubingwa. Arsenal wataingia msimu huu wakilenga kutetea taji lao, huku ushindi dhidi ya Manchester City ukiweza kuwa mwanzo muhimu wa safari hiyo. Soma Zaidi: Meli ya kivita ya Marekani yaelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya USS Abraham Lincoln Meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani imeanza safari kuelekea Mashariki ya Kati kuchukua nafasi ya meli ya USS Abraham Lincoln, ambayo maelfu ya mabaharia wake wameripotiwa kukabiliwa na uhaba wa chakula na mazingira magumu ya maisha wakati wa operesheni yake ya miezi tisa. Kulingana na uchunguzi wa BBC, meli ya USS George Washington, iliyokuwa karibu na Malaysia siku ya Alhamisi, huenda ikafika katika eneo hilo ndani ya takriban siku tisa. Familia za baadhi ya mabaharia wa USS Abraham Lincoln zimeelezea wasiwasi kuhusu kudorora kwa afya ya akili ya jamaa zao kutokana na hali ngumu wanayokabiliana nayo, huku kukiwa na ripoti za baadhi ya mabaharia wakitaka kujirusha ndani ya bahari. Jeshi la Wanamaji la Marekani limekubali kuwepo kwa matatizo ya usambazaji wa mahitaji muhimu kwa wanajeshi hao, lakini limekanusha kuwa wanajeshi hao wanakabiliwa na changamoto za afya ya kiakili. USS Abraham Lincoln, ina takriban wanajeshi 5,000. Akizungumza na waandishi wa habari hapo jana, Rais wa Marekani Donald Trump alipuuzilia wasiwasi ambao umetolewa na familia za wanajeshi walioko katik meli hiyo ambao wanadai muda wa oparesheni ya meli hiyo imekuwa ndefu sana. Soma pia: Watu wanne wauawa katika shambulizi la makombora la Wahouthi nchini Yemen Serikali ya Yemen imewalaumu kundi la wapiganaji la Wahouthi kwa kurusha makombora sita ya kibalistiki katika bandari ya Mocha, kwenye Bahari ya Shamu, hapo jana na kuwaua watu wanne. Kulingana na maafisa wa serikali ya Yemen, shambulizi hilo lililenga miundombinu ya kiraia na maeneo ya bandari, huku boti kadhaa za uvuvi zikichomwa moto. Kwa upande mwingine, Wahouthi wamesema katika taarifa yao kuwa walilenga vituo vya kijeshi, silaha na ndege za vikosi vinavyoungwa mkono na Saudi Arabia huko Mocha, kwa kuwarushia makombora. Tukio hili limetokea wakati mvutano unaendelea kutokota eneo hilo kati ya Wahouthi na Saudi Arabia, Pamoja na mvutano kati ya Marekani na Iran. Soma pia: 'Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa na utaendelea kuwa wa Iran' - Kazem Akijibu kauli ya Rais wa Marekani Donald Trump ya kutangaza Mlango wa Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani, Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amesema kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.” Kazem Gharibabadi alichapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X na kusisitiza kuwa “Mlango wa Bahari wa Hormuz hauwezi kutekwa kupitia ujumbe uliochapishwa kwenye X au meli ya kubeba ndege za kivita.” Waziri huyo aliongezea kuwa Iran “haiogopi vitisho wala maonyesho ya nguvu.” Gharibabadi pia alidai kwamba “Marekani hadi sasa imepata kushindwa katika mikakati yake ya vita.” Kulingana naye, “Iran pekee ndiyo yenye mamlaka ya kufunga au kufungua Mlango wa Bahari wa Hormuz.” Soma pia: Trump atishia kutangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba hivi karibuni atatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa sehemu ya eneo la Marekani, akidai kuwa Iran imeathirika vibaya na vita vilivyotokea eneo hilo. “Baada ya kuishinda Iran, ambayo sasa imeathirika vibaya,hivi karibuni nitatangaza Mlango Bahari wa Hormuz kuwa eneo la Marekani,” Trump alisema katika mkutano wa kisiasa mjini New York. Kauli ya Trump imekuja wakati mkwamo unashuhudiwa kati ya Washington na Tehran kuhusu mlango huo wa bahari. Mlango Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ambayo hupitisha kiasi kikubwa cha mafuta na bidhaa tofauti duniani. Iran imeweka udhibiti katika sehemu kubwa ya mlango huo, na kuzuia meli nyingi za mizigo za kiraia kupita, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likiweka kizuizi katika bandari za Iran katika jaribio la kudhoofisha uchumi wa nchi hiyo. “Tumeweka kizuizi. Hakuna meli itakayopita isipokuwa sisi wenyewe tutake ipite,” Trump aliwaambia wafuasi wake. Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Kazem Gharibabadi, amejibu kauli ya Trump mapema hii leo kupitia mtandao wa X na kusema, “Mlango huu wa bahari hautafunguliwa wala kufungwa isipokuwa kwa amri ya Iran, na msipo kubali ukweli kuwa mmeshindwa, mtaendelea kujidanganya, na Iran itaendelea kuweka kizuizi.” Gharibabadi alisisitiza kuwa Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kumilikiwa na Iran, “Mlango Bahari wa Hormuz ulikuwa wa Iran, ni wa Iran, na utaendelea kuwa wa Iran.” Soma pia: Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja

How it works

Once you click Generate, Ollama reads this article and crafts 5 comprehension questions. Your answers are graded against the article content — general knowledge won't be enough. Score 70+ to count toward your certificate.

Questions are cached — you'll always get the same 5 for this article.